Timu ya taifa ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza
kuonyesha uhodari na umahiri wao katika mchezo wa mieleka baada ya
kuibwaga timu ngumu ya Russia kwenye mchezo wa fainali wa kombe la dunia
kwa mtindo wa freestyle, baada ya kuibanjua kwa ushindi wa 6 -1, kwenye
uwanja wa Azadi mjini Tehran.
Ikishangiliwa na nyomi za washabiki elfu
kumi na mbili waliofurika uwanjani na wakati wote wa mashindano
walikuwa wamesimama wima, huku wakitoa vifijo, nyemi, na hoihoi za
nderemo za Iran, Iran, Iran na kuwatia morali wanamieleka wa timu ya
taifa ya Iran ambao hatimaye walijipatia medali sita za dhahabu katika
uzani wa kilo 55, 60, 74, 84, 96 na 120. Hali kadhalika Iran ilijipatia
medali ya fedha katika uzito wa kilo 66. Russia iliyoshika nafasi ya
pili, iliambulia medali moja ya dhahabu katika uzito wa kilo 66 na
medali nyingine sita za fedha.Timu ya mieleka ya Marekani ilishika nafasi ya tatu na kujizolea medali za shaba baada ya kuibwaga Belarus kwa 6-1. Naye Mkuu wa Shirikisho la Mieleka la Marekani amesema kuwa, watazamaji wa Iran wameuthibitishia ulimwengu kwamba, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC ilifanya makosa kwa kuchukua maamuzi ya pupa ya kuufuta mchezo wa mieleka kwenye mashindano ya Olimpiki ya 2020.






0 comments:
Post a Comment